Rubani wa ndege iliyoanguka Nepal hakuripoti hatari yoyote kabla ya ajali

0
12

Msemaji wa uwanja wa ndege wa Pokhara, Anup Joshi amesema rubani wa ndege ya Yeti Airlines iliyoanguka ikitokea Mji Mkuu wa Nepal uitwao Kathmandu Jumapili hakuripoti chochote cha hatari wakati ndege hiyo ikikaribia uwanja wa ndege.

Anup amedai upepo ulikuwa wa kawaida na hakukuwa na shida ya hali ya hewa, na kuwa rubani wa ndege aliomba kubadilishwa kutoka barabara ya tatu iliyopewa hadi ya kwanza ambayo ilikubaliwa na uwanja wa ndege, na ndege hiyo ikaruhusiwa kutua.

Baadhi ya video ziliionesha ndege hiyo iliyokuwa na watu 72 ikiyumba sana ilipokuwa ikikaribia uwanja wa ndege na kugonga ardhi kwenye korongo la Mto Seti, zaidi ya kilomita moja kutoka uwanja wa ndege.

Afisa wa eneo hilo, Tek Bahadur amesema uwezekano wa kumpata mtu yeyote akiwa hai ni hafifu huku mpaka sasa miili 68 ikipatikana pamoja na vinasa sauti.

Waziri Mkuu wa Nepal ametangaza Jumatatu kuwa siku ya kitaifa ya maombolezo, pia Serikali imeunda jopo la kuchunguza chanzo cha maafa hayo.