Rubi ya Tanzania inayopigwa mnada Dubai yazua utata

0
23

Wizara ya Madini imesema haina taarifa yoyote kuhusu jiwe la rubi kuonekana katika maonesho ya vito yaliyoandaliwa na Kampuni ya SJ Gold and Diamond huko nchini Dubai.

Akizungumza na Gazeti la Mwananchi kuhusiana na taarifa hiyo, Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema wizara haina taarifa yoyote kuhusu jambo hilo, hivyo watafuatilia na kutoa majibu.

“Tunafuatilia jambo hili, hawa watu wangeeleza ukweli hii rubi imetoka wapi. Lakini hadi Jumatano ya wiki ijayo tutajua, maana hata aliyepeka hatumjui,” amesema Biteko.

Maonyesho hayo yanayojulikana kama Callisto Collection yanafanyika leo nchini humo na kuipa nafasi dunia kujionea rubi hiyo nyekundu inayodaiwa kuwa na thamani ya TZS bilioni 276 za Kitanzania.

Rubi hiyo iliyochimbwa katika Kijiji cha Winza wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma itapigwa mnada baada ya kumalizika kwa maonesho hayo na mfungo wa mwezi wa Ramadhani.