Rushwa ya ngono yatawala uhamisho na upangaji vituo vya kazi kwa walimu

0
43

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imebaini kughubikwa na vitendo vya rushwa ya ngono katika upangaji wa vituo vya kazi kwa waajiriwa wa idara ya elimu.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthness Kibwengo akitoa taarifa kuhusu utendaji wa taasisi hiyo, amesema TAKUKURU imefanya uchambuzi katika mifumo sita ikiwemo mfumo wa elimu na kubaini uwepo wa mianya ya rushwa katika sekta hiyo.

“Tumebaini kuwa maeneo hatarishi ya uwepo wa rushwa ya ngono ni katika upangaji wa vituo vya kazi kwa asilimia 72,” amesema Kibwengo.

Aidha ameeleza kuwa eneo lingine hatarishi kwa uwepo wa rushwa ya ngono ni eneo la uhamisho wa walimu ndani ya halmashauri hiyo ambayo ni kwa asilimia 63.

Hata hivyo ameongeza kuwa taasisi hiyo imefuatilia utekelezaji wa miradi 41 ikiwemo sekta ya ujenzi, afya, maji na elimu yenye thamani ya shilingi bilioni 11.2 na kubaini miradi 10 ina upungufu ikiwemo vifaa viinavyotumika kutokidhi ubora.