Ruto amuonya Kenyatta kwa kufadhili maandamano kwa siri

0
37

Rais wa Kenya, William Ruto amempa onyo mtangulizi wake Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta kuhusu madai ya kushirikiana na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kuipinga Serikali.

Rais Ruto amedai Uhuru amekuwa akifadhili kwa siri maandamano ya Odinga dhidi ya serikali ambayo hivi karibuni yameleta matokeo mabaya ikiwa ni pamoja na vifo vya raia, na kubainisha kuwa iwapo atashindwa kusitisha ufadhili huo hatua zitachukuliwa dhidi yake.

“Nataka nimwambie rafiki yangu Uhuru, hata wewe achana na huyu mzee (Odinga), acha kumpatia pesa ya kununua watu wa Mungiki wachome Nairobi. Wewe umekuwa Rais, kuwa mungwana. Tulikuunga mkono wakati ulikuwa Rais wetu, ulimuunga mkono tukamwangusha, achana na yeye,” amesema.

Rais Samia: Nchi za jirani zinatamani fursa tuliyoipata

Ameongeza, “usipoachana na yeye, ata wewe tutakusafirisha na huyo ‘kitendawili wako’. Uhuru Kenyatta tulimsaidia akiwa Rais, sasa anapanga kuchoma Nairobi, imemkosea nini?”

Aidha, Rais Ruto amesema ingawa kufanya maandamano ni haki ya raia yeyote kama ilivyoainishwa kwenye katiba, lakini hatua za kisheria zitachukuliwa kwa Odinga ikiwa umwagaji damu zaidi utashuhudiwa katika mchakato huo.

Odinga amekuwa akiongoza mamia ya Wakenya kufanya maandamo ili kupinga Serikali ya Rais William Ruto kutokana na hali ngumu ya maisha na kupinga baadhi ya maamuzi ya Serikali hiyo.

Send this to a friend