Rais wa Kenya, William Ruto amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga, na yuko tayari kutoa ustahimilivu katika masuala ambayo yatasaidia maendeleo ya taifa.
Ametoa kauli hiyo wakati wa ibada ya kanisa Kaunti ya Kwale siku ya Jumapili, ambapo amesema alikutana na kiongozi wa upinzani na timu yake wiki hii.
Hata hivyo, Ruto ametoa sharti kwa upinzani kabla ya mazungumzo ambayo yatasimamiwa na aliyekuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo ambapo ametaja sharti hilo kwamba hakuna kiongozi yeyote atakayepanga maandamano ya vurugu nchini tena.
“Nilizungumza na kiongozi wa upinzani [Raila] na timu yake, nikawaambia kuwa sisi ni nchi ya kidemokrasia inayofuata katiba na sheria. Tunaweza kutokubaliana katika masuala mengi lakini hakuna kiongozi wa sasa, wa zamani au wa baadaye atakayepanga vurugu au uharibifu wa mali. Hilo halitatokea tena Kenya,” amesema.
Ameongeza kuwa “Tumeafikiana kuwa vurugu na uharibifu wa mali hautakuwa sehemu ya siasa na utawala wa Kenya. Mambo mengine tunaweza kuzungumza,” aliongeza.