Ruto awaonya maafisa wa polisi juu ya mauaji ya raia

0
16

Rais wa Kenya, William Ruto amewaonya maafisa wa polisi dhidi ya mauaji ya kiholela ya waandamanaji wanaoipinga serikali, huku upande mwingine akisisitiza kwamba kila mtu lazima afuate sheria zilizowekwa.

Akizungumza katika ziara yake katika Kaunti ya Murang’a, Ruto ameshikilia msimamo wa serikali yake kukabiliana na wavunja sheria iwe katika vyombo vya usalama au hadharani kuhusiana na maandamano yanayoendelea yakiongozwa na upinzani.

Amerejea ahadi yake ya kutokomeza utovu wa nidhamu na kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa na kuongeza kuwa ataleta utulivu nchini humo na hakuna mtu atakayeruhusiwa kusababisha ghasia, fujo na uharibifu wa mali.

“Tunaomba maafisa wetu wa kusimamia sheria wawe waangalifu, wasimame na ninataka kupongeza vyombo vyetu vya usalama kwa kuwa na weledi wa jinsi ambavyo vimewashughulikia watu hawa. Wahalifu lazima washughulikiwe kwa uthabiti na kuhakikisha kwamba kila mtu anaheshimu utawala wa sheria.”

Ruto amuonya Kenyatta kwa kufadhili maandamano kwa siri

Akizungumzia kuhusu maafisa wa usalama kushutumiwa kutumia nguvu kupita kiasi kwa waandamanaji, Rais amesema wanafanya kazi yao ya kuhakikisha kuwa nchi hiyo inakuwa na amani na utulivu bila kuangalia mamlaka aliyonayo mtu.

Aidha, amewahakikishia Wakenya kwamba waandamanaji wanaoongozwa na chama cha Azimio la Umoja One Kenya hawataharibu mpango wake wa kiuchumi kwa nchi huku akiwataka Wakenya kuwa watulivu.

“Tutahakikisha Kenya iko salama, sisi ni nchi ya demokrasia, amani, hatutaki fujo, vita kwa sababu hatuna muda wa kupigana. Kama raia tunataka muda wa kufanya kazi katika uchumi na kukuza nchi yetu.”

Send this to a friend