
Rais wa Kenya, William Ruto ameshangazwa na watu kumtaka aondoke madarakani mapema, akisema kuwa hata yeye atamaliza muda wake na kuondoka kama viongozi waliomtangulia.
Kauli hiyo ni kufuatia kuongezeka kwa kaulimbiu ya ‘Ruto Must Go’ kupitia maandamano ya mitaani na mitandao ya kijamii ambapo vijana mara kwa mara wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa ya maisha, kodi, ukosefu wa ajira, ufisadi serikalini na sera tata za serikali.
“Kama waliokuwepo kabla yangu, muda wangu utafika na nitaondoka. Lakini kwa heshima, ndugu na dada zangu, sababu zenu za kusema ‘Ruto must go’ ni zipi?” ameuliza.
Ameongeza, “Pengine hamkubaliani na mipango yangu kwa taifa, hilo ni sawa. Lakini tafadhali, tupeni mpango mbadala. Ninaposikiliza zaidi, naona ni maneno tu ya kauli bila maudhui.”








