
Rais wa Kenya, William Ruto ameahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha kuwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga anaheshimiwa ndani na nje ya nchi hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya UDA na ODM katika KICC siku ya Ijumaa, Rais ameeleza kuwa wenzake, walio chini yake, na hata wakubwa wake wanapaswa kutambua mchango wa Raila ambao umedumu kwa vizazi kadhaa.
“Miezi kadhaa baada ya uchaguzi, nilimwambia kuwa amekuwa kiongozi wangu wa chama, na nataka aheshimiwe ipasavyo. Nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuhakikisha kuwa unapata heshima nchini Kenya. Sifanyi hivi kwa sababu za kibinafsi, bali ni kwa sababu wewe ni mkongwe wangu na mchango wako unastahili kuheshimiwa,” alisema.
Muda mfupi baada ya viongozi hao wawili kusaini makubaliano ya ushirikiano, Ruto amebainisha kuwa makubaliano hayo yameonesha jinsi watu binafsi wanavyoweza kuweka maslahi ya taifa mbele kuliko maslahi yao binafsi.
“Mpangilio huu si kuhusu kugawana vyeo au kushinda uchaguzi, bali ni kuhusu maslahi ya Wakenya. Ni wakati wa sisi kuungana kama taifa,” amesisitiza.
Aidha, amempongeza Odinga kwa juhudi zake za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), akisema kuwa Raila amejijengea heshima kama mpiganiaji wa bara la Afrika.