Rwanda yafunga makanisa zaidi ya 10,000

0
73

Serikali ya Rwanda imefunga zaidi ya makanisa 10,000 kwa kushindwa kutimiza masharti ya sheria ya mwaka 2018 inayodhibiti maeneo ya ibada nchini humo.

Sheria hiyo iliweka masharti mapya kuhusu afya, usalama na uwazi wa kifedha, na pia inamtaka kila mhubiri kuwa na mafunzo ya theolojia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Paul Kagame amesema haoni mchango mkubwa wa baadhi ya makanisa katika kutatua changamoto za dunia kama vile vita na ukosefu wa ajira. Amesema badala ya kusaidia jamii, yapo makanisa yanayotumiwa kama njia ya kujinufaisha binafsi.

Agosti mwaka huu zaidi ya makanisa 4,000 yalifungwa baada ya kushindwa kutimiza masharti ya afya na usalama. Bodi ya Utawala ya Rwanda ilieleza kuwa kuongezeka kwa kasi kwa baadhi ya makanisa kunachochewa na waanzilishi wanaotafuta faida binafsi, ikiwemo fedha na mali kutoka kwa waumini, huku wakieneza mafundisho ya kupotosha.

Rais Kagame amehimiza taasisi za kidini kujikita zaidi katika kuchangia elimu, afya na maendeleo ya kijamii badala ya kujiingiza katika shughuli za kibiashara, akisisitiza kuwa imani ya dini inapaswa kuwainua watu, na si kuwafanya maskini.

Send this to a friend