Rwanda yatafakari kuitoza kodi Netflix

0
30

Mamlaka nchini Rwanda zinatafakari uwezekano wa kutoza kodi kwenye huduma za mtandao, tovuti ya New Times imeeleza ikimnukuu mmoja wa maafisa kutoka mamlaka inayohusika na ukusanyaji kodi.

Kodi hiyo ya ongezeko la thamani inayopendekezwa kutozwa imetajwa kuwa ni ya muhimu katika kupanua wigo wa vyanzo vya mapato.

“Unapolipia huduma kama Netflix, unatumia fedha ambazo umezipata nchini Rwanda. Hivyo, tunajiuliza, kwanini tusikusanye VAT kwenye huduma hizi kama zinalipiwa wa raia wetu,” amehoji Jean-Louis Kaliningondo kutoka Mamalaka ya Mapato Rwanda (RRA).

Kusudio la Rwanda linakuja wakati mjadala sawa na huo unaendelea kushika kasi mitandaoni nchini Tanzania, baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira kuhoji kwanini wanaofanya biashara mitandaoni hawalipi kodi kama walivyo wafanyabiashara wengine.

Hata hivyo, hoja yake ilipingwa na Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akisema kwamba biashara ya mtandao nchini bado ni changa sana na inahitaji kutunzwa na kukuzwa kwani vijana wengi wamejiajiri kupitia kwayo.

Mwaka 2021 Kenya ilianzisha Kodi ya Huduma za Kidijitali (DST) ambapo iliweka tozo ya 1.5% kwenye thamani ya huduma au bidhaa itakayouzwa kwenye jukwaa la kidijitali.

Send this to a friend