Rwanda yazindua kiwanda kikubwa cha kutengeneza simu (smartphones)
Kampuni ya Mara Group inayomilikiwa na mfanyabiashara Ashish J. Thakkar imefungua kiwanda cha teknolojia ya juu cha kutengeneza simu katika ukanda wa kiuchumi jijini Kigali, nchini Rwanda.
Kiwanda hicho ambacho kilizinduliwa jana na Rais Paul Kagame kina uwezo wa kuzalisha simu milioni 2 kwa mwaka. Akizungumza katika uzinduzi huo, Thakkar alisema kiwanda hicho kinakusudia kutengeneza simu zenye ubora wa juu zitakazouzwa kwa bei nafuu ili kuwezesha lengo la kuboresha ukuaji wa matumizi ya simu za kisasa barani Afrika.
Miaka michache iliyopita tulitambua kuwa ili kuleta matokeo chanya kwenye jamii yetu katika bara la Afrika, na katika masoko yanayokuwa, tunahitaji kuwa na simu zenye ubora wa juu, zinazopatikana kwa bei nafuu. Hapo ndipo tulipopata wazo la Mara Phones, alisema Thakkar wakati wa ufunguzi.
Nchini Rwanda asilimia 15 tu ya wananchi ndio wanaotumia simu janja (smartphones), ambapo nyingi kati ya hizo ni Tecno na Samsung.
Kiwanda cha Mara Phones kitaanza kuzalisha aina mbili za simu ambazo ni Mara X na Mara Z. Simu zote zitauzwa chini ya $200 (TZS 460,000), ambapo pamoja na mambo mengi itakuwa na betri inayoweza kudumu muda mrefu, uwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa. Kampuni hiyo pia imeingia ubia na taasisi za kifedha na mitandao ya simu nchini humo, ambapo mnunuaji wa simu anaweza kulipa kidogo kidogo kwa hadi miaka miwili. Hapa chini ni muonekano wa moja ya simu zitakazozalishwa na kiwanda hicho:
Mara Group imesema kiwanda hicho ndiyo kikubwa cha chenye teknolojia ya juu zaidi barani Afrika. Thakkar amesema viwanda vingi vilivyopo Afrika si vya kutengeneza simu, bali kuunganisha (assembling plants), lakini walichofungua nchini Rwanda ni kiwanda cha kutengeneza simu.
Kiwanda hicho tayari kimetoa ajira kwa watu 200, ambapo wanawake ni asilimia 60 ya nguvu kazi yote.
Mara Phones inatarajia kufungua kiwanda kingine cha kutengeneza simu mwishoni mwa mwezi huu nchini Afrika Kusini.
Ashis Thakkar (38) ni mwanzilishi wa Mara Group, kampuni yenye makazi yake Dubai, ambayo inaangazia soko la Afrika ikitoa huduma mbalimbali kama vile teknolojia, huduma za kifedha, uzalishaji, viwanda vya kilimo, huduma za nyumba na mashamba (real estate).