Sababu 6 za kwanini mtoto wako analia kwa muda mrefu usiku

0
55

Baadhi ya wazazi huchukulia hali ya kawaida kwa watoto wao kulia nyakati za usiku, huku wengine wakiihusisha na imani mbalimbali bila kujua kuwa hali hiyo inaweza kuchangiwa na baadhi ya mambo ambayo yanaweza kurekebishwa.

Kwa mujibu wa Daktari ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mohammed V cha nchini Morocco, Peter Kyoba anabainisha baadhi ya mambo ambayo huchangia mtoto kulia zaidi wakati wa usiku.

Njaa

Njaa inaweza kuwa chanzo cha mtoto kulia sana wakati wa usiku kwa sababu kupitia chakula ndipo anaweza kuendana na mahitaji ya mwili wake katika ukuaji.

Gesi kujaa

Sababu nyingine ni gesi kujaa tumboni, mara nyingi hali hiyo humfanya mama kulalamika kuwa mtoto anajinyonga, ili kuepuka hali hiyo mama anashauriwa kumcheulisha mtoto kila baada ya kumnyonyesha pamoja na kumweka vizuri wakati anapokuwa ananyonya.

Kulowa kwa nepi

Endapo mtoto hatobadilishwa nepi kwa muda mrefu inaweza kumfanya kulia kwa muda mrefu hasa nyakati za usiku, hivyo wazazi wanashauriwa kuwa makini na kuwaweka watoto wao katika hali ya usafi na ukavu wakati wote.

Mabadiliko ya hali ya hewa

Kipindi cha joto au baridi kinaweza kuchangia mtoto kulia sana usiku. Endapo kuna joto sana unashauriwa kumpunguzia mtoto nguo, na kama ni kipindi cha  baridi hakikisha unamvalisha nguo nzito na kumfunika vizuri.

Kutokuoga usiku

Inaelezwa kuwa kutomuogesha mtoto usiku kunaweza kumfanya mtoto kushtuka shtuka usiku hivyo kuchangia kulia mara kwa mara.

Maumivu ya tumbo

Kwa maelezo ya Daktari Ford Chisongela kutoka Hafford Clinic anasema mtoto mdogo asiye na njaa wakati mwingine hulia kutokana na maumivu ya tumbo.

“Ikiwa analia kwa zaidi ya saa tatu kwa siku, siku tatu kwa wiki au kwa zaidi ya wiki tatu hali hii ni fumbo kigo. Wataalamu wanakubaliana kuumwa tumbo kwa watoto wachanga kunaanza karibu na umri wa wiki mbili kama mtoto alizaliwa amekomaa (siyo njiti),  tatizo linaweza kuanza baadaye ikiwa alizaliwa kabla ya wakati (njiti),” ameeleza Chisongela.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend