Mwili wako una vinyweleo ambavyo ni vifuko vidogo vilivyo na seli maalum za rangi ambazo huzingira nywele. Seli hizi za rangi zinaitwa melanini. Melanini huipa ngozi na nywele zako rangi. Muda unavyozidi kusonga, vinyweleo hivi vya nywele hupoteza rangi na kusababisha mvi.
Nini hupelekea kuota mvi katika umri mdogo?
Sababu za kijenetiki
Kwa baadhi ya watu suala la nywele kubadili rangi huwa la kiukoo. Ikiwa wazazi au babu zako walikumbwa na tatizo hili, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba wewe pia utapitia hali hiyo. Kwa bahati mbaya, hakuna jambo ambalo linaweza kufanyika ili kuepuka.
Msongo wa mawazo
Kila mtu hukabiliana na msongo wa mawazo mara kwa mara. Matokeo ya msongo yanaweza kujumuisha matatizo ya usingizi, wasiwasi, mabadiliko ya hamu ya kula na shinikizo la damu. Ikiwa umeona kuongezeka kwa idadi ya nywele nyeupe, msongo wa mawazo unaweza kuwa chanzo.
Upungufu wa virutubisho vya vitamini
Ukosefu wa virutubisho vya kutosha vya vitamin B12 mwilini pia vinaweza sababisha ngozi na nywele kubadilika rangi. Aidha, upungufu huu unaweza kusababisha hali ya upungufu wa damu mwilini.
Masuala ya homoni
Iwapo tezi dundumio (thyroid gland) haifanyi kazi ipasavyo, huenda uwezo wa mwili wako kuzalisha melanini ukapungua na hivyo kusababisha nywele zako kubadili rangi mapema. Tezi dundumio ni kikoromeo kidogo kinachopatikana katika sehemu ya mbele ya shingo lako.
Maradhi yanayotokana na mwitiko wa kinga usio wa kawaida
Katika hali hii, mfumo wa kinga mwilini hushambulia seli zake. Kuna aina mbili katika kitengo hiki; ‘alopecia areata’ na ‘vitiligo’ ambazo zinaweza kusababisha nywele kubadili rangi mapema.
Uvutaji sigara
Uvutaji sigara una madhara mengi ikiwa ni pamoja na saratani, maradhi ya moyo na mapafu. Uvutaji sigara unaweza kuhusishwa na kuota kwa mvi.
Rangi za kemikali na bidhaa zingine za nywele
Bidhaa za nywele zilizoundwa kwa kemikali ya ‘hydrogen peroxide’ zimeonekana kuwa na madhara kwa nywele na zinaweza kusababisha kuota kwa mvi.
Sababu zinazopelelezwa
Kuna utafiti unaohusisha tatizo la nywele kubadili rangi mapema na wembamba wa mifupa (osteopenia) na maradhi ya moyo, lakini upelelezi zaidi unafanyika.