Sababu kuu tatu za Sumaye kujitoa CHADEMA

0
24

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye leo Disemba 4, 2019 ametangaza rasmi kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kuwa ndani ya chama hicho kwa miaka minne na miezi minne.

Sumaye ambaye alitikisa vichwa vya habari alipong’atuka Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga CHADEMA Agosti 2015 ili kuipa nguvu dhana ya mabadiliko iliyokuwa kaulimbiu ya vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), amesema kwamba safari yake ndani ya CHADEMA imetamatika leo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Sumaye ametaja sababu mbalimbali zilizomsukuma yeye kujiondoa ndani ya CHADEMA ambazo ni pamoja na figisu katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani.

Sumaye ambaye alikuwa akishikilia nafasi hiyo amesema kuwa chama hicho kiliwalipa wajumbe wa mkutano ili wampigie kura za hapana, huku baadhi ya wajumbe wengine wakifichwa hotelini wasiende kupiga kura.

Kama wakubwa wameamua kuwashawishi wapiga kura wangu wa Kanda ya Pwani hata kwa kuwaficha Hotelini, hii maana yake naambiwa Sumaye akufukuzae akuambii toka

Katika uchaguzi huo Sumaye ambaye alikuwa ndiye mgombea pekee, tena anayetetea nafasi hiyo alipata kura za hapana 48, kati ya kura 76, na hivyo akapoteza nafasi hiyo. Amesema kuwa jambo hilo haliingii akilini kwani wajumbe hao ndio walimuomba agombee, lakini hao hao wapige kura nyingi za hapana, jambo ambalo linaonesha kuwa njama zilipangwa kuhakikisha kuwa hachaguliwi.

Sababu nyingine amesema kuwa ni mchakato wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, ambapo amebainisha kuwa mchakato huo sio wa kidemokrasia kama wengi wanavyoweza kudhani. Amesema kwamba, wakati anakwenda kwenye uchaguzi wa kanda, tayari alikuwa amechukua fomu ya uenyekiti taifa, na hiyo ni moja ya sababu zilizopelekea yeye kufanyiwa figisu akose uongozi wa kanda.

Amebainisha kuwa, sababu ya yeye kuchukua fomu ya taifa ilikuwa kuuonesha ulimwengu kuwa ndani ya CHADEMA kuna demokrasia, na sio kama watu wanavyodhani kuwa nafasi ya uenyekiti taifa ni ya Freeman Mbowe tu. Kama CHADEMA kwao nafasi ya mwenyekiti hauguswi basi wanginiambia kuliko haya waliyofanya, amesema Sumaye.

Akitangaza uamuzi wa kujitoa CHADEMA ameweka wazi kuwa sababu nyingine ni usalama wake, usalama wa familia yake pamoja na chama hicho.

Katika kipindi chote cha uchaguzi amesema familia yake imekuwa ikipata usumbufu mkubwa sana, na anaamini kwa yeye kutoka CHADEMA na kutojiunga na chama kingine cha siasa (kwa sasa), familia yake itapumzika.

Labda kwa kitendo hiki mke wangu na wanangu watanivalisha taji kwa kuwaondolea adha walizokuwa wanapambana nazo kwa mimi kuwa upinzani. Jambo jema tuheshimiane na tuheshimu utu wa mtu.

Katika maelezo yake yote, Sumaye ameonesha kutoridhishwa na hali ya demokrasia ndani ya chama hicho na kusema kuwa lengo la kujiunga cha chama hicho ilikuwa ni kutengeneza upinzani wenye nguvu utakaoshindana na CCM, lakini kwa hali ilivyo sasa mchakato huo amesema utachukua muda mrefu sana.

Amesema anafahamu kuwa Mbowe atakuwa mwenyekiti wa chama hicho, na amesihi kuhakikisha anavunja makundi yaliyopo ndani ya chama na kujenga umoja ambao utakiimarisha chama hicho.

Licha ya kutoka CHADEMA, amesema kuwa ana imani cha chama hicho na ataendelea kushirikiana nacho katika kuimarisha demokrasia kama kitamhitaji, huku akisisitiza kuwa ni lazima baadhi ya mambo ndani ya chama hicho yabadilishwe.

Send this to a friend