Sababu ya wananchi kupata ‘unit’ za umeme tofauti kwa kiwango sawa cha fedha

0
101

Watumiaji mbalimbali wa umeme wamekuwa wakilalamikia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutokana na utofauti unaojitokeza katika viwango vya ‘unit’ za umeme wanazopata pindi wanaponunua umeme kwa kiwango sawa cha fedha.

Mfano, watu wawili wanaweza kununua umeme wa TZS 10,000 na wasipate viwango sawa vya unit. Mmoja anaweza kupata unit 28 wakati mwingine akapata zaidi ya hizo.

Swali kubwa ambalo wengi hujiuliza kwanini hali hiyo hutokea. Jibu lake, ni kwa sababu kuna utofauti wa kiwango cha matumizi ya umeme.

Bei ya umeme inatofautiana kutokana na kundi la matumizi mteja alilopo, mfano matumizi madogo ya nyumbani (D1) ambao wanatumia umeme wa majumbani na matumizi yao ni wastani wa KWh 75 kwa mwezi wananunua umeme uniti moja kwa Tsh 100 (bila kodi). Endapo watazidi hapo kila unit watatozwa Tsh 350 (bila kodi).

Lakini, kwa wateja wa kundi la matumizi ya kawaida (T1), kundi hili hujumuisha wateja wenye matumizi ya kawaida ya umeme hususani watumiaji majumbani, biashara na viwanda vidogo, taa za barabarani na mabango. Hawa wananunua umeme unit moja Tsh 292 (bila kodi), kundi hili linatumia kuazia unit 75-7500 kwa mwezi.

Hivyo kutofautiana kwa kundi la matumizi ndicho kinachopelekea wateja kupata units tofauti kwa kiasi kilekile cha fedha. TANESCO ndio wanafahamu mteja fulani anatakiwa kuwa katika kundi fulani.