Sababu za aliyekuwa waziri nchini Gambia kuhukumiwa miaka 20 jela

0
39

Mahakama Kuu ya Uswizi Mei 15, 2024 imemhukumu Ousman Sonko (55), Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa Gambia, kifungo cha miaka 20 jela kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa makosa yaliyorekodiwa kati ya mwaka 2000 na 2016, enzi za utawala wa Rais Yahya Jammeh.

Ousman Sonko ni nani?
Ousman Sonko alizaliwa Januari 9, 1969 nchini Gambia katika Mji wa Serekunda ulio karibu na Pwani ya Atlantiki, kilomita 13 kutoka Mji mkuu Banjul.

Mwaka 1988 Sonko alijiunga na jeshi la Gambia, kisha akajiunga na walinzi wa serikali ambao walikuwa na jukumu la kumlinda Rais. Februari 2005 alipandishwa cheo cha juu zaidi katika jeshi la Gambia kama Inspekta Jenerali (IGP).

Kuanzia Novemba 2006 hadi Septemba 2016, alishika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Gambia. Kupandishwa kwake cheo kuwa waziri kulikuja kwa sababu ya uaminifu wake alipokuwa Mkuu wa Polisi wa Jammeh hadi alipoondolewa madarakani na kukimbia Gambia.

Kwanini Sonko alishtakiwa?
Septemba 2016 katika miezi ya mwisho ya utawala wa Jammeh, Sonko alituma maombi ya kukaa nchini Uswisi lakini akanyimwa. Inaaminika alihamia Uswisi, ambako alikamatwa katika kituo cha wanaotafuta hifadhi mnamo Januari 2017.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAG) ya Uswisi ilimfungulia mashtaka Aprili 2023 kwa makosa mengi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu lakini Sonko alikana madai dhidi yake.

Kesi yake ilianza kusikilizwa Januari 8, 2024 katika mahakama ya shirikisho nchini Uswisi. Miongoni mwa makosa ya uhalifu aliyoshtakiwa kwayo ni pamoja na mauaji ya mwaka 2000 ya Almamo Manneh, mwanajeshi aliyeshukiwa kufanya mapinduzi, mke wa Manneh pia alimshutumu Sonko kwa kumbaka mara nyingi baada ya kuuawa kwa mumewe.

Mashtaka mengine ni mauaji ya Oktoba 2011 ya Baba Jobe, mbunge wa zamani wa Bunge la Gambia, na ukandamizaji mkali wa mkutano wa kisiasa mjini Banjul mwezi Aprili 2016, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kukusudia ya Ebrima Solo Sandeng, mmoja wa waandaaji wa mkutano huo, na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria na kuteswa kwa wanachama kadhaa wa upinzani.

Imeelezwa kuwa Sonko alikuwa na dhima ya kusimamia mashambulizi ya kupangwa yaliyotekelezwa na vyombo vya usalama vya Gambia kwa lengo la kuwanyamazisha wapinzani wa utawala wa Jammeh.

Send this to a friend