Sababu za mtu kukoroma anapolala, na namna ya kuepuka

0
60

Kukoroma ni sauti inayotolewa na mtetemo wa tishu za koromeo unaosababishwa na kupungua kwa misuli ya njia ya upumuaji wakati mtu akiwa usingizini.

Wapo wanaokoroma wanapolala chali endapo wametoka kunywa pombe au kutumia dawa, pia wapo wanaokoroma kutokana na mabadiliko ya kianatomia, kuvuta sigara, mimba na historia ya magonjwa ya mzio.

Rais wa chama cha usingizi nchini Brazili na mratibu wa huduma ya matatizo ya usingizi, Edilson Zancanella anasema kubadilisha namna ya kulala na kupumzika kwa misuli huathiri mtiririko wa hewa.

Inakadiriwa kuwa, karibu nusu ya watu wazima duniani wanakoroma, na pia mtoto mmoja kati ya 10 anakoroma pia.

Mtaalamu wa magonjwa ya mapafu, Luciane Mello amewahi kusema kuwa kukoroma ni ishara ya onyo au dalili mbaya kwamba njia ya hewa imezuiliwa au imepunguzwa ukubwa.

Mambo 5 yatakayokusaidia kulala vizuri usiku

Mbali na athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, wataalamu wanashauri pia kuchunguza uwepo wa patholojia kama vile apnea ya kuzuia usingizi, kuziba kwa njia ya hewa kwenye koo ambayo husababisha mtu kuacha kupumua kwa muda.

Namna gani ya kuzuia kukoroma?

Kwa wale wanaokoroma kidogo au kutokana na kuziba kwa pua kutokana na mafua, kubadilisha namna ya kulala kunaweza kupunguza au kutatua tatizo.

Mabadiliko ya mtindo wa maisha pia yanapendekezwa kama vile kupunguza uzito, kuacha kuvuta sigara na matibabu ya mizio na magonjwa ya kupumua, kufanya mazoezi ambayo huimarisha muundo wa koo kunaweza kusaidia kupunguza au kuondoa kabisa hali hii.