Sababu za Rais Samia kutunukiwa Udaktari wa Heshima na chuo kikuu India

0
42

Chuo Kikuu maarufu nchini India cha Jawaharlal Nehru, leo Oktoba 10, 2023 kimemtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (Doctorate Honoris Causa), Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo na chuo hicho.

Rais Samia anapokea shahada hiyo ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kumtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari kutambua mchango wake katika kuboresha sekta ya elimu, uchumi, demokrasia, na usawa wa kijinsia nchini.

Chuo hicho kilianzishwa Aprili 22, 1969 na kupewa jina la Waziri Mkuu wa kwanza wa India, Jawaharlal Nehru, na kuwa moja ya vyuo vikuu bora nchini India na duniani kwa ujumla kikijivunia kuwa taasisi ya elimu ya juu ambapo watu maarufu wa India walipata elimu yao ya juu.

Baadhi ya majina maarufu yaliyoandikishwa katika chuo hicho ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Bw. Subrahmanyam Jaishankar, na Waziri wa Fedha, Bi. Nirmala Sitharaman, huku kikitoa Shahada ya Heshima kwa viongozi wawili pekee akiwemo Rais wa Urusi, Vladmir Putin pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan, Hayati Shinzo Abe.

Shahada hiyo ya heshima imetolewa kwa kutambua juhudi za Rais Samia katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na India, kutokana na mafanikio yake katika uwanja wa kidiplomasia, haswa diplomasia ya kiuchumi, na mafanikio katika kuchochea maendeleo yanayojikita kwa watu nchini Tanzania.

Aidha, sababu nyingine ni kutokana na mafanikio yake katika kuendeleza ushirikiano wa kikanda, kuimarisha mahusiano ya kimataifa, na kuendeleza utaratibu wa kushirikiana kimataifa katika Umoja wa Mataifa.

Send this to a friend