Sabaya asomewa mashtaka mapya saba
Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imemsomea mashtaka saba aliyekuwa Mkuu wa Waya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne.
Sabaya na wenzake wamesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Salome Mshasha na chini ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka wakishtakiwa kwa makosa yakiwemo kuendesha genge la uhalifu, kupokea rushwa, utakatishaji wa fedha pamoja na ukiukwaji wa mamlaka ya utumishi.
Kweka amesema katika shtaka la kwanza linalowahusu washtakiwa wote, inadaiwa Sabaya akiwa Mkuu wa wilaya ya Hai alikiuka majukumu yake ya kiutendaji kwa makusudi na kwa nia ya kutekeleza jinai na kujipatia shilingi milioni 30.
Aidha, katika shtaka la rushwa, kwa nia ya kuzuia taarifa za uchunguzi zinazohusiana na ukwepaji wa kodi imeelezwa kuwa Februari, 2021 Sabaya alishawishi na kuomba rushwa ya shilingi milioni 30 kutoka kwa Godbless Swai katika eneo la Bomang’ombe wilayani Hai pamoja na kupokea rushwa ya shilingi milioni 30 kutoka kwa Elibariki Swai.
Akijibu malalamiko ya wakili wa utetezi, Hellen Mahuna aliyedai mahakamani hapo kuwa taratibu za kuwafikisha wateja wake mahakamani hazikufuatwa, Hakimu Salome amesema hakuna kifungu cha sheria kinachoilazimisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kupata kibali kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwani tayari Mahakama ya Moshi ilishaandika barua katika Gereza la Kisongo ili washtakiwa hao kuletwa gereza la Karanga Moshi.