Safari ya maisha ya Charles Hilary: Redio Tanzania hadi Ikulu (Zanzibar)

0
16

Leo Desemba 30, 2021 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amemteua Charles Hilary kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano – Ikulu.

Mambo mengi yanaweza kuandikwa kuhusu mkongwe huyo mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 36 katika tasnia ya  habari akiwa amefanya kazi katika vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.

Tutaangazia kwa uchache yanayomhusu. Charles alizaliwa Zanzibar miaka 62 iliyopita eneo la Jang’ombe.

Mwaka 1968 alihamia jijini Dar es Salaam na kujiunga na Shule ya Msingi ya Ilala Mchikichini.

Alijiunga na Redio Tanzania mwaka 1981 na kukitumikia chombo hicho cha umma hadi mwaka 1994 alipojiunga na kituo binafsi cha Radio One Stereo kinachomilikiwa na IPP.

Mwaka 2003 aliondoka nchini na kujiunga na Radio Deusch Welle nchini Ujerumani, na miaka mitatu baadaye alijiunga na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akiwa Idhaa ya Kiswahili.

Mwaka 2015 alirejesha mpira kwa kipa baada ya kuamua kurejea nchini na kujiunga Azam Media. Alieleza sababu za kuondoka BBC kurejea nchini kuwa ni umakini wa wamiliki wazawa wa vyombo vya habari.

Miongoni mwa rekodi zake na kwamba yeye ndiye Mtanzania wa kwanza kutangaza kwa Kiswahili mechi za fainali za Kombe la Dunia (mwaka 2010) akiwa uwanjani.

Redio nyingi ziliwahi kutangaza fainali hizo kwa Kiswahili, lakini zote zilifanya hivyo kwa kuangalia mechi hizo kwenye runinga na si kutokea uwanjani.

Anakumbukwa sana kwa uhodari wake wa kutangaza mpira na kipindi cha Charanga Time kilichomzidishia umaarufu akiwa Radio One Stereo.

Pamoja na  mambo memgine yaliyowahi kumsibu, aliwahi kunusurika kuuawa kwa risasi mwaka 1964, siku moja baada ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoundoa utawala wa Sultan na kuiweka Serikali ya Watu wa Zanzibar.

Charles alikutwa na tukio hilo Januari 13 wakati akiwa na umri wa miaka mitano.

Send this to a friend