Saikolojia: Namna 5 za kupunguza wasiwasi unaokuzonga wakati huu wa coronavirus

0
36

Janga la homa ya kirusi cha corona (COVID-19) linaendelea kuisumbua dunia huku idadi ya walioambukizwa ugonjwa huo ikizidi kuongezeka ambapo hadi leo asubuhi ilikuwa zaidi ya watu milioni mbili. Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeliita janga la kidunia, nchi matajiri zinataabika huku maelfu wakipoteza maisha na kuna sintofahamu nyingi hasa kutokana na ukweli kwamba ni kirusi kipya, hakina tiba na watafiti wa magonjwa bado wako katika maabara kujaribu kukielewa sawasawa. Wataalamu wa saikolojia wanasema kwamba, katika hali tete namna hii ni hulka ya binadamu wote kuwa na wasiwasi, wala si jambo la kushangaza.

Mwanadamu hukumbwa na hofu litokeapo jambo ambalo hana hakika kwamba anaweza kupigana nalo na kulishinda. Sifa ya binadamu ni siku zote kujaribu kuwa na control na yanayomzunguka. Hiyo humpa amani, lakini inapotokea hali ambayo hana nguvu hiyo basi wasiwasi huchukua nafasi.

Lakini tunaambiwa kwamba katika kipindi hiki wasiwasi na woga waweza kuleta athari kubwa zaidi hata ya kirusi chenyewe cha korona. Mfano wataalamu wa tiba wanaeleza kuwa wasiwasi huleta msongo wa mawazo ambayo huathiri kinga ya mwili, na kinga ya mwili hii ndiyo silaha namba moja ya kushindana na kirusi anayevamia mwili. Hivyo basi wasiwasi unaanza kuua uwezo wako wa kupambana na kirusi hata kabla hujakipata kirusi chenyewe. 

Katika makala hii fupi kwa msaada wa majarida ya tiba ya kimataifa kuna orodha ya hatua chache ambazo unaweza kufuata ili kusaidia kubaki imara kiafya ya akili na kuondoa msongo wa mawazo katika muda huu kitu ambacho ni hatari. 

1. Punguza kiasi cha taarifa unachosoma kuhusu coronavirus 

Wanasaikolojia wanapendekeza ukizidisha sana utumie dakika 30 kwa siku kusoma habari, mitandao ya kijamii, na taarifa mitandaoni. Pia wanapendekeza kujaribu kila wiki kutenga wala siku moja nzima bila kupekua mitandao ya kijamii na intaneti kutafuta habari.

Mtandaoni kuna mamilioni ya taarifa kuhusu coronavirus lakini chache zina manufaa na bahati mbaya hutaweza kusoma zote na kufahamu zipi sahihi, zipi si sahihi. Kadiri unavyojaza kichwa chako na taarifa lukuki kuhusu jambo hili ndivyo wasiwasi unavyoongezeka na athari kwa mfumo wako wa kinga ya mwili zinaanza.

2. Wekeza akili yako kwa mambo ambayo unaweza kuyabadili tu

Usipoteze muda kwenye mambo ambayo kwa hakika huyawezi. Mfano kuwaza dawa ya coronavirus wakati wewe si mtafiti wa tiba za virusi. Kwa nini unawaza? Itasaidia nini? Tiba ikipatikana hakika utapata taarifa. Fuata maagizo ya mamalaka rasmi za afya. Mfano: 

  • Nawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni walau kwa sekunde 20 au tumia kitakasa mikono (sanitizer)
  • Kaa mbali na wagonjwa
  • Vaa barakoa (mask) lakini kipaumbele kama ziko chache wapewe watu ambao tayari wana maambukizi, wahudumu wa afya, wazee na watu wenye kinga dhaifu ya mwili. 
  • Epuka kushika uso wako kadiri inavyowezekana
  • Kuwa na umbali kati yako na watu wengine walau futi 6 au mita 2 mnapokutana (ikiwa ni lazima sana mkutane)
  • Epuka safari zisizo za lazima kwenda popote 
  • Weka kinga yako ya asili ya mwili sawa kwa kula vizuri, kulala vizuri na kuepuka stress zisizo za msingi

Mambo haya tunayaweza, hivyo basi bora kuyafanya na kuwa mtazamo chanya kwamba umefanya sehemu yako kwa yale unayoyaweza.

3. Jiweke bize na mambo mengine 

Hii ni mbinu ya zamani lakini isiyochuja ya kupambana na wasiwasi na msongo wa mawazo.

Mfano sikiliza muziki unaopenda, pigia simu wapendwa wako, kaa na familia au mwenzi, lala, tazama muvi, na kadhalika. This is a classic tactic for keeping anxiety under control. 

4. Zungumza na mtu ambaye unajisikia amani kuzungumza naye 

Hawa ni watu ambao kwenye maisha huwa tunajisikia faraja kuzungumza nao kuhusu wasiwasi wetu kwenye maisha. Huwa ni watu ambao hatuna wasiwasi kwamba watatu-judge. Watu ambao unajua huyu huwa ananisikiliza na kunishauri vizuri na kunifanya nisikie amani.

Tofauti na kwenda mtandaoni na kuomba ushauri kwa kila mtu na kupokea maoni ambayo yanatoka kwa watu wasiokufahamu na pengine yatakuumiza zaidi na utapagawa zaidi.

5. Tumia muda katika imani yako ya kidini kama unayo

Binadamu ni kiumbe ambaye asipokuwa na majibu ya jambo mikononi mwake basi hujaribu kupata faraja kwa kuelezea shida hiyo kwa nguvu ya uumbaji (Mungu/God/Allah/Maulana, n.k.) kupitia sala na maombi.

Kisaikolojia wako wengi waliopata amani ya moyo kwa kusali na kuomba ulinzi wa Muumba hivyo basi hii ni njia mojawapo ambayo inapendekezwa katika kuondoa msongo wa mawazo na wasiwasi.

Baki Salama!

Robi Sagati, UDSM, BA in Psychology (Year 3)

sagati.robi@gmail.com

Send this to a friend