Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa Meneja wa TEHAMA wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Lonus Feruzi na wasaidizi wake Frank Mushi na Idda Njau, hadi hapo uchunguzi kuhusu kukosekana kwa huduma ya LUKU kukosekana utakapokamilika.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo mkoani Dar es salaam kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati wa kikao chake na Menejementi pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO.
Waziri Mkuu amesema kuwa kuwasimamisha siku 10 tu haitoshi, kwani siku 10 zikipita na uchunguzi haujakamilika watarudi kazini, jambo ambalo haliwezi kukubalika.
“Lazima tufundishane kuwa makini, kila siku lazima tukague vifaa vyetu ili huduma ipatikane muda wote. Hakuna kuwasimamisha kwa siku 10, wakae pembeni hadi timu inayochunguza itakapotoa matokeo. Inawezekana sio wao tu, waziri endelea na uchunguzi,” ameagiza Waziri Mkuu.
Aidha, ameiagiza TANESCO kuhakikisha inakuwa na mfumo mbadala (backup) ambao utakaotumika pindi kunapotokea changamoto za kimfumo, ili kuepusha adha kwa wananchi kama ambavyo imekuwa kwa siku kadhaa.
“Mmetengeneza usumbufu mkubwa sana, mlijua lazima kuwe na backup lakini hakuna, toka pale tulipoanza kutoa huduma mpaka leo kwanini hakuna backup, hilo ni jukumu lenu,” amesema Waziri Mkuu.
Huduma ya LUKU kielektroniki imekosekana kwa siku kadhaa nchini, na hivyo kuwalazimu wanaohitaji huduma ya umeme kufika katika ofisi za TANESCO mikoani na wilayani ambako kulikuwa na misururu ya watu.