Sakata la milioni 602 za bwawa, Aweso awasimamisha kazi wanne

0
26

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewasimamishwa kazi watumishi wanne wa wizara hiyo kufuatia kusuasua kwa kazi ya ujenzi wa Bwawa la Kwankambala wilayani Handeni.

Akitoa maagizo hayo Aweso ameelekeza pia kushikiliwa kwa Mkandarasi Civil Loth Enterprises Ltd kwa hatua za uchunguzi baada ya kugundulika kuwa aliondoa vifaa vya kazi katika eneo la ujenzi, licha ya kwamba ilikuwa imeongezewa muda wa utekelezaji wa ujenzi.

Hatua hizo zimechukuliwa baada ya kufanya ziara ya kikazi wilayani Handeni Aprili 12, 2022, ambapo ilibainika mkandarasi anayejenga bwawa la Kwankambala amelipwa kiasi cha TZS milioni 602.8, sawa na asilimia 33 ya gharama ya mkataba huku kazi iliyofanyika ikiwa ni asilimia 20 ya kazi zilizopangwa kufanyika.

Watumishi waliosimamishwa (ambao wote ni kutoka RUWASA Makao makuu) ni Msimamizi wa Mradi Hamisi Matungulu, Mhasibu Mkuu, CPA Jimmy Mwanyakunga, Meneja Udhibiti Ubora wa Miradi na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi, Amos Mtweve na Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugav, Zam Mlimira.

Pamoja na hayo waziri amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kuunda tume ya uchunguzi ili kubaini changamoto zinazokabili utekelezaji wa mradi.

Send this to a friend