Sakata ndege za ATCL lachukua sura mpya, waishitaki Airbus wakitaka fidia

0
43

Sakata la ndege mbili za Airbus A220 za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutofanya kazi limefika katika Shirikisho la Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA) ili kupatiwa ufumbuzi.

Hayo yamejiri baada ya ndege hizo kushindwa kufanya kazi tangu Oktoba mwaka jana kutokana na sababu za hitilafu ya injini huku kampuni iliyotengeza ndege hizo kushindwa kuwa na injini za ziada na kupelekea hasara kwa wateja wake ikiwemo ATCL.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amebainisha kuwa wanaendelea kuwabana watengenezaji wa ndege hizo kwa kushirikiana na mashirika mengine barani Afrika zenye umiliki wa ndege za aina hiyo.

Mfumuko wa bei washuka Februari 2023

“Kwa kweli hili ni tatizo, lakini tunaendelea kuwabana, kwa sasa tunashirikiana na mashirika mengine yanayotumia ndege kama hizo, likiwemo la Air Senegal, Misri ili kututatulia tatizo hili kwa haraka,” amesema.

Aidha, amesema watengenezaji hao wanatakiwa kuwalipa ATCL fidia ambayo ipo kwenye mkataba, “lakini imechukua muda mrefu sasa, na sasa imekuwa si suala la fidia bali wameharibu biashara na kulifanya shirika kupoteza mapato.”

Ameeleza kuwa ufumbuzi wa tatizo hilo ni kupatiwa injini nyingine au ndege zitakazotumika katika kipindi kifupi wakati wao wakiendelea kutatua changamoto hiyo kupata injini ya ziada.

ATCL ina ndege 12 kati ya hizo ndege zake tatu hazifanyi kazi kwa sababu za kiufundi zikiwemo Airbus mbili zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 120 na 160.

Send this to a friend