Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL), moja ya viwanda vikubwa vya bia nchini, iliyokamilisha mwaka wake wa fedha mwezi Juni, imebainisha kuwa kampuni hiyo imetumia kiasi cha Tzsh bilioni 12 kwa jamii za Watanzania katika kununua nafaka, huku ikiweka mikakati ya kushirikiana na wakulima wadogo wengi zaidi wilayani Handeni, mkoa wa Tanga, ambapo kampuni hiyo imeanza kuandikisha wakulima wilayani humo kuanza kulima mtama ambao kampuni hiyo itanunua kwa ajili ya uzalishaji.
Mradi huo ambao unatarajiwa kuanza mwakani, SBL itakuwa na jumla ya mikoa nane ambayo inachukua malighafi zake, huku kampuni hiyo ikiwa na mipango ya kuongeza mikoa mingine ikiwemo Mbeya na Bukoba. Kwa sasa, SBL inapata malighafi zake kutoka mikoa saba, yaani; Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Iringa, Singida, na Shinyanga.
Kama sehemu ya maandalizi ya awali ya mradi huu, wakulima wilayani Handeni tayari wameanza kusajiliwa kushiriki katika mradi huu uliosubiriwa kwa hamu, huku ekari 658 za ardhi zikitengwa kwa ajili ya mradi ambao utajumuisha mashamba ya majaribio. Mradi huu unatarajiwa kuleta manufaa kwa wakulima wa Handeni, kwa kuzingatia kipaumbele kutolewa kwa wanawake na vijana. Mradi huu utaimarisha zaidi azma ya SBL ya kuongeza ukusanyaji wa malighafi zake kutoka kwa wakulima wadogo hadi kufikia asilimia 85, ambayo ni sawa na tani 13,000 ifikapo mwaka 2024 kutoka asilimia 70 ya sasa, ambayo ni sawa na tani 11,000.
Uwekezaji wa SBL kwa wakulima wadogo ni sehemu ya nguzo muhimu ya kampuni hiyo inayojulikana kama ‘Kutoka Nafaka hadi Glasi’. Katika kutekeleza nguzo hii, SBL inashirikiana kwa karibu na wakulima wadogo si tu kupata malighafi kutoka kwao bali pia kuwawezesha kiuchumi.
Hadi sasa tumeshirikisha jumla ya wakulima 400 katika mikoa saba ambapo tayari tuna kanzidata ya wakulima tunavyofanya nao kazi, kwa mfano katika mwaka wa fedha uliopita tumenunua jumla ya tani 11,000 za malighafi yetu kutoka kwa wakulima wadogo katika mikoa saba ambayo tayari ipo kwenye kanzidata yetu. Hii ni ongezeko la 70% ikilinganishwa na 65% ambayo tulipata kutoka kwao mwaka wa fedha uliopita,” alisema Meneja wa Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Rispa Hatibu.
Akizungumzia kuhusu mradi wa kilimo cha mtama uliokusudiwa katika wilaya ya Handeni, Hatibu alisema SBL imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Afisa Kilimo wa Wilaya, Yibarila Kamele, kutambua maeneo yanayofaa kwa mradi huo, pamoja na kuwasajili wakulima wadogo wa Handeni ili washiriki katika mradi huo wa kilimo cha mtama.
Kwa upande wake, Kamele alisema, “Awali, tulikuwa tumepanga wakulima waanze kulima mwaka huu lakini tukaona kwamba msimu huu hautatupatia matokeo bora, kwa hiyo, nilipendekeza utekelezaji wa mradi uanze mapema mwaka ujao, hii itawapa wakulima nafasi ya kuandaa mashamba yao vizuri kwa ajili ya mradi huu.”
Hatibu aliendelea kusema kuwa, kampuni hiyo ya kutengeneza pombe inatarajia kuongeza idadi ya wakulima wadogo kutoka 400 wa sasa hadi 700 ifikapo mwaka 2025, ambapo kutahusisha kuongeza mikoa zaidi ikiwa ni pamoja na Tanga, Mbeya, na Kagera.
Kupitia nguzo ya SBL “From Grain to Glass,” uwekezaji wa kampuni katika wakulima wadogo unajumuisha kutoa mbegu pamoja na mafunzo ya kiufundi kwa wakulima, ili kuwawezesha kufanya kilimo endelevu.