Sefue, Mukandala wateuliwa kusimamia taasisi za serikali

0
52

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi kama ifuatavyo:-

Wenyeviti wa Bodi/Baraza la Chuo:

• Amemteua Balozi Ombeni Y. Sefue kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Balozi Sefue anachukua nafasi ya Bwana Halfani Ramadhani Halfani. Balozi Sefue ni katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu.

• Amemteua Bwana Halfani Ramadhani Halfani kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA);

• Amemteua Prof. Rwekaza Sympho Mukandala kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Prof. Mukandala anachukua nafasi ya Bi. Gaudentia Kabaka. Prof. Mukandala ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mstaafu.

• Amemteua Prof. Saida Yahaya Othman kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Mzumbe. Prof. Othman anachukua nafasi ya Prof. Mathew Laban Luhanga ambaye alifariki dunia tarehe 16 Septemba, 2021. Prof. Othman ni Mhadhiri Mstaafu (retired Associate Professor) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

• Watendaji Wakuu wa Taasisi:

• Amemteua Mhandisi Charles Jimmy Sangweni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), kabla ya uteuzi huu Mhandisi Sangweni alikuwa anakaimu nafasi hiyo.

• Amemteua Mhandisi Modestus Martin Lumato kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). Kabla ya uteuzi huu Mhandisi Lumato alikuwa Meneja Uzalishaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

• Amemteua Bwana Eliachim Chacha Maswi kuwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA). Bwana Maswi anachukua nafasi ya Dkt. Irene Charles Isaka ambaye anakwenda kutumikia wadhifa wa Mkurugenzi wa Huduma za Jami (Director of Social Sector) katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Uteuzi huu unaanza mara moja.

Send this to a friend