Sekta Binafsi yabadilisha sura ya Bandari ya Dar es Salaam

0
2

Baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kufanya uamuzi wa kuruhusu Sekta Binafsi katika uendelezaji na uendeshaji wa baadhi ya maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam ikiwemo Kampuni ya Dubai ya DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL), serikali imesema mafanikio makubwa yameanza kuonekana.

Bandari ya Dar es Salaam iliyokuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi, hivi sasa imeanza kuleta tija mbalimbali ikiwemo kupungua kwa gharama za uendeshaji wa bandari hiyo kutoka Shilingi bilioni 975.01 hadi kufikia Shilingi bilioni 685.16 sawa na punguzo la asilimia 30.

Akizungumza bungeni wakati wa uwasilishaji wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawe amesema licha ya kupungua kwa gharama za uwendeshaji, mapato yatokanayo na Kodi ya Forodha kutokana na shughuli za kibandari, yameongezeka kwa shilingi trilioni 1.18.

“Katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Februari, 2025 jumla ya Shilingi trilioni 8.26 zimekusanywa sawa na ongezeko la Shilingi trilioni 1.18 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 7.08 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2023/24 kabla ya kushirikishwa kwa Waendeshaji binafsi katika bandari hiyo,” amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, muda wa kusubiri meli nangani umeelezwa kupungua kutoka wastani wa siku 46 hadi wastani wa siku saba kwa meli za mizigo mchanganyiko na kichele, na meli za makasha gatini kutoka wastani wa siku 10 hadi siku tatu.

Prof. Mbarawa amesema matokeo ya uendeshaji wa bandari hadi kufikia mwezi Machi, 2025 tayari ufanisi wa uhudumiaji wa shehena wa bandari zote nchini umefikia tani milioni 27.55 na kwa mwenendo huo lengo la tani milioni 30 litafikiwa mapema sana kabla ya muda uliowekwa.

Kampuni ya DP World ilianza uendeshaji wa shughuli za bandari ya Dar es Salaam mwezi Aprili, 2024 kwa kipindi cha miaka 30, ambapo kampuni hiyo chini ya Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu, Sultan Ahmed Bin Sulayem ilisema itawekeza dola milioni 250 [TZS bilioni 674.5] ndani ya miaka mitano.

Send this to a friend