Sensa itakavyowezesha ukusanyaji tozo za majengo

0
52

Tanzania inatarajia kufanya sensa ya watu na makazi Agosti 2022, ambapo miongoni mwa manufaa ya ni kufahamu idadi na aina ya nyumba zilizopo nchini, hatua ambayo itaweka urahisi katika ukusanyaji wa kodi ya majengo.

Licha ya kwamba zoezi hilo hufahamika kama Sensa ya Watu na Makazi, lakini kwa sensa zilizopita hazikuhusisha ukusanyaji wa taarifa za nyumba.

Hayo yameeleza na Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizundua Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, leo Septemba 14,2021 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

“Tangu tumepata uhuru nchi yetu haijawahi kufanya sensa ya majengo. Licha ya kwamba zilizopita zilikuwa zinaitwa sensa za watu na makazi lakini hatukuwa tukichukuwa idadi ya majengo na makazi ya watu,” amesema Rais Samia na kuongeza kuwa taarifa hizo zitawezesha pia utekelezaji wa mradi wa makazi.

Aidha, Rais ameeleza kuwa sensa hiyo itawezesha kukusanya anuani za makazi ya wananchi, hivyo kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali, na endapo mtu aliyechukua mkopo asipolipa, serikali itaweza kujua alipo.

Sensa ya mwakani itakuwa na utofauti na mwaka 2012 kwani kutakuwa na kutenga maeneo ya kijiografia ya kuhesabia watu katika ngazi za kitongoji/mtaa na upatikanaji wa taarifa za kitakwimu katika ngazi za kitongoji/mtaa pamoja na kuwa na mipaka ya kudumu katika ngazi hizo, matumizi ya Vishikwambi (tablets) katika hatua zote za utekelezaji wa sensa kwa lengo la kupunguza gharama na nyongeza ya maswali yatakayowezesha upatikanaji wa taarifa zaidi za kitakwimu ikilinganishwa na Sensa ya Mwaka 2012.

Send this to a friend