Serekali kugharamia matibabu ya Prof. Jay

0
44

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali itagharamia gharama zote za matibabu ya aliyekuwa mbunge wa Mikumi, Mwanamuziki Joseph Haule, maarufu Professor Jay, mpaka pale atakaporuhusiwa na madaktari.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati alipomtembelea Haule Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufikisha salamu hizo kutoka kwa Rais Samia.

“Nimefika kuleta salamu za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu, ambaye yupo safarini nje ya nchi. Amesema kuwa anatambua mchango wa Prof. Jay akiwa Mbunge wa Mikumi lakini pia kazi zake za sanaa ambazo zimehamasisha vijana wengi kujiajiri kupitia muziki, hivyo kuanzia sasa  Serikali itagharimia matibabu yake hadi hapo atakaporuhusiwa kutoka hospitalini, na ninauagiza uongozi wa hospitali kuleta bili zote wizarani kuanzia sasa,” amesema Waziri Ummy

Pia ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango wa Pro. Jay kwenye jamii kupitia sanaa yake, na Rais anatoa pole kwa familia yake kwa kuuguza,  na anamtakia kila la kheri katika matibabu yake pia anamuombea apone haraka ili aendelee na shughuli zake.

 Bi Grace Mgonjo ambaye ni  mke wa Prof. Jay amemshukuru Rais na kusema kuwa amefanya jambo kubwa sana kwa familia yake na kuongeza kuwa hawajajutia kufuata matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Ninashukuru sana Uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kwa kuwa tangu tulipofika hapa walitupokea vizuri sana na hatujawahi kujutia kuwa hapa” amesema Bi Grace.

Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu amewapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kazi kubwa wanayoifanya katika utoaji wa matibabu ya kibingwa yanayotolewa kwa Watanzania na kuahidi kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika kufanya kazi.

 

Send this to a friend