Serikali imesema bajeti ya Sensa ya Watu na Makazi, na Sensa ya Majengo ambayo iliidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni kiasi cha TZS bilioni 400, sawa na wastani wa shilingi 6,265 kwa mtu mmoja.
Hayo yamesemwa leo Agosti 31, 2022 na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kuhusu maendeleo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi hadi kufikia Agosti 31, 2022.
Aidha, amebainisha jumla ya majengo yaliyokwisha hesabiwa kuwa ni 6,351,927 ambapo taarifa za umiliki, mahali yalipo na taarifa zingine zilizoainishwa katika dodoso la majengo zimekusanywa.
Taarifa hiyo inasema, hadi kufikia Agosti 31,2022 kiwango cha watu waliohesabiwa nchi nzima kimefikia asilimia 99.93, hivyo kubaki kiwango cha asilimia 0.07 ya kaya zote nchi nzima, na kwamba asilimia hizo zilizobaki zitahesabiwa hadi kufikia Septemba 5 mwaka huu.