
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imesema kuwa watumishi wapato 15,288 walioondolewa katika utumishi wa umma kwa kosa la kughushi vyeti wameshalipwa michango yao yenye jumla ya shilingi bilioni 47.02 na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSF.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi hiyo ni kufuatia habari zilizochapishwa na moja ya chombo cha habari kuwa maelekezo aliyoyatoa Rais Samia Suluhu katika sherehe za Mei Moi mwaka 2022 jijini Dodoma, juu ya kurejeshewa michango yao watumishi hao hayatekelezeki.
Watumishi waliokuwa wakichangia katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) walistahili kurejeshewa michango ya asilimia tano, na waliokuwa wakichangia NSSF asilimia 10.
CHADEMA yaeleza sababu za kutosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi
Ofisi hiyo imesema kufuatia maelekezo ya Rais, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma alitoa maelekezo kupitia barua yenye kumbukumbu CFC. 26/205/01″AT”/20 ya tarehe 31 Oktoba, 2022 kwa waajiri wote katika taasisi za umma kutekeleza maelekezo ya Rais, ambapo maelekezo hayo yametekelezwa kwa ufasaha na uadilifu.
“Ofisi hii imesikitishwa na habari zilizoandikwa katika gazeti hilo kwani hazina ukweli wowote, na kwa mtazamo wetu zimelenga kuwachafua viongozi na jina la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na kuleta taharuki,” imeeleza Ofisi hiyo.