
Serikali imesema hadi Aprili 2025, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 107.70 ambapo kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni 72.94 na deni la ndani ni shilingi trilioni 34.76.
Akisoma Bajeti Kuu bungeni, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Oktoba 2024 imeonesha kuwa deni ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
“Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa kwa mwaka 2024/25: thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 23.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180,” amesema.
Ameongeza kuwa “Matokeo ya tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa yanaendelea kuipa taswira chanya nchi yetu katika medani za kimataifa. Matokeo hayo ni bora kuliko nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.”
Amesema pamoja na mambo mengine, matokeo hayo yamechangiwa na jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta binafsi, kukuza uchumi, kusimamia kwa makini deni la Serikali na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.