Serikali: Gharama halisi za kuunganisha umeme mijini na vijijini ni takribani 800,000
Waziri wa Nishati, January Makamba amesema gharama halisi ya kuunganisha huduma ya umeme kwenye nyumba kwa wakazi wa mijini na vijijini ni takribani Shilingi laki nane.
Akizungumza kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, Makamba amesema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ili kupunguza gharama hiyo kwa kutambua umuhimu wa umeme na maisha halisi ya Watanzania.
“Mwananchi akitakiwa kulipa Shilingi 27,000 ajue Serikali inachangia Shilingi 773,000 kutoka kwenye mfuko wake, na tukisema mteja alipe Shilingi 321,000 kwa kiwango hicho ajue Serikali inachangia Shilingi 489,000, ni muhimu lijulikane hili,” amesema Waziri Makamba.
Ameongeza kuwa gharama za umeme na gharama za kuunganisha umeme zinapangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) hivyo, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) haliwezi kutoza gharama nje ya kiwango kilichopangwa na mamlaka husika.