Serikali haitatangaza ikipandisha mishahara ya watumishi

0
38

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewatoa hofu watumishi wa umma kuhusu maslahi yao na kubainisha kuwa serikali haitatangaza hadharani itakapopandisha mishahara yao.

Ameyasema hayo bungeni leo akijibu swali la mbunge aliyetaka kufahamu kauli ya serikali kuhusu lini itapandisha mishahara ya watumishi wa umma kwani kwa muda mrefu wamekuwa wavumilivu na wakiwa na matumaini ya mishahara yao kupandishwa.

Akieleza sababu za uamuzi wa kutotangaza, amesema wakati serikali inaingia madarakani ilibaini kuwa nyongeza ya mishahara inapotangazwa hadharani inapelekea kupanda kwa gharama za maisha na hivyo kuathiri makundi mengine ambayo si ya watumishi.

“Tuna wafanyakazi tuna wakulima tuna wafugaji tuna wavuvi, hayo ni makundi mbalimbali. Kwa wafanyakazi pekee ukitangaza kuwa umepandisha mishahara, kwenye masoko yetu, vituo vya mabasi na huduma nyingine zote zinapanda,” ameeleza Majaliwa.

Aidha, amesema kuwa serikali imekuwa ikiboresha maslahi ya wafanyakazi, na kueleza kuwa maslahi hayapo tu kwenye mishahara kwani kwa kuwapandisha vyeo, kupunguza kodi kutoka tarakimu mbili hadi moja, kunakuwa na tija zaidi kuliko kuongeza TZS 10,000 kwenye mishahara yao.

Amesema serikali inatambua mchango wa watumishi katika maendeleo ya taifa na hivyo waendelee kuchapa kazi kwani serikali ina makusudi ya dhati ya kuboresha maslahi yao.

“Wafanyakazi wetu tuendelee kufanya kazi, tuendelee kuiamini serikali na tuendelee kutumia vyombo vyetu kwa maana jumuiya zetu za wafanyakazi ili kuendelea kuzungumza maeneo yanayohitaji kufanyiwa kazi kwa lengo la kuleta maslahi kwa wafanyakazi,” amehitimisha waziri mkuu.

Send this to a friend