Serikali: Hakuna kampuni ya simu yenye leseni ya kutoa mikopo

0
48

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema kwa mujibu wa sheria za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hakuna kampuni ya simu iliyopewa leseni ya kutoa mikopo kwa wananchi, hivyo wananchi waepuke mikopo yenye masharti magumu maarufu kama ‘Kausha Damu’ na badala yake watumie taasisi zenye leseni za kutoa mikopo.

Akijibu swali la mbunge aliyeuliza kuwa ni lini kampuni za simu zitalazimishwa kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutoa mikopo, amesema ili kampuni, taasisi au mtu binafsi aweze kutoa mikopo kwa wananchi anapaswa kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania na kukidhi matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha.

“Kampuni za simu zinazotoa huduma za fedha zimepewa leseni ya kutoa huduma za mifumo ya malipo kulingana na matwaka ya sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015 pamoja na kanuni zake,” ameeleza.

Ameongeza kuwa “mikopo inayotolewa na benki na taasisi za fedha kupitia mifumo ya kampuni za simu ni kama ilivyoanishwa hapo awali. Mikopo iliyopata umaarufu wa kuitwa ‘Kausha Damu’ hutolewa na taasisi ambazo hazina leseni ya Benki Kuu ya Tanzania

Aidha, amesema Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kuzuia mikopo hiyo ikiwa ni pamoja na kuzitaka kampuni za simu kuhakikisha mifumo yao haitumiki katika shughuli zozote zinazohusiana na mikopo hiyo pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waepukane na kuchukua mikopo hiyo.

Send this to a friend