
Serikali imesema kwa kutambua mabadiliko ya kisera kutoka kwa baadhi ya washirika wa muda mrefu wa masuala ya UKIMWI, serikali inachukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuimarisha uwekezaji kwenye eneo la utoaji huduma kwa wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU)
Akisoma hotuba ya ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa Fedha 2025/2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hatua hizo zenye lengo la kuwezesha taifa kujitegemea, zitaendelea kuchukuliwa pia katika maeneo mengine.
“Niwahakikishie Watanzania wote, kuwa, serikali itaendelea kuhakikisha huduma zinazohusiana na masuala ya UKIMWI zinaendelea kupatikana na hakuna Mtanzania hata mmoja atakayekosa huduma hizo,” amesema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuratibu shughuli za UKIMWI kwa kutoa huduma endelevu na stahimilivu kwa WAVIU kwa kuimarisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ili uweze kufanikisha malengo ya nchi katika kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030.
Serikali: Watu 60,000 wanaambukizwa VVU kila mwaka
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka msukumo katika kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika jamii ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu ametoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa UKIMWI bado ni tishio nchini.