Serikali: Hatutazuia safari za usiku za mabasi ya ‘hakuna kulala’

0
25

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Zuberi Homera imesema serikali haitapiga marufuku mabasi madogo ya abiria yanayofanya safari zake usiku maarufu ‘hakuna kulala’ kwa madai kuwa itachangia kushusha uchumi wa mkoa wa huo.

Badala yake Homera ameiagiza mamlaka husika kutoa vibali kwa magari yanayofanya safari hizo ikiwa ni siku chache tangu Kamanda wa Kikosi Cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa kuonya vitendo vya kufanya safari kinyume na utaratibu.

“Mabasi ya ‘hakuna kulala’ yataendelea kufanya safari huku tukiweka utaratibu wa makubaliano baina ya wamiliki kuingia mkataba na Jeshi la Polisi kwa kupatiwa ulinzi usiku ili kulinda usalama wa raia na mali zao,” amesema Homera.

Awali Kamanda Mutafungwa alionya safari hizo kutokana na vijana tisa wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe kupoteza maisha baada ya basi dogo aina ya Coaster kugongana uso kwa uso na lori aina ya Howo wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.

Akizungumzia suala hilo la vibali, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (LATRA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Denis Daudi amesema wamepokea agizo hilo la utoaji wa vibali kwa mabasi ya ‘hakuna kulala’ na kwamba wanasubiri maagizo kutoka ngazi za juu.

Send this to a friend