Serikali kuanzisha kambi maalumu kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema Serikali, kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), inajipanga kuanzisha kambi maalumu za mawakili watakaotembelea magereza yote nchini kwa lengo la kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa.
Akizungumza leo tarehe 14 Desemba 2024, wakati wa ziara yake katika Gereza la Kiberege, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro, Waziri Ndumbaro amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mmoja, hususan kwa wafungwa na mahabusu wenye changamoto mbalimbali za kisheria.
“Kambi hiyo itaanzia hapa Gereza la Kiberege ambapo mawakili wa TLS watajizatiti kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa. Hii ni moja ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha kuwa mfumo wa haki unawafikia wote kwa usawa,” alisema Waziri Ndumbaro.
Ziara hiyo pia ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya ‘Mama Samia Legal Aid Campaign,’ inayolenga kutoa msaada wa kisheria bila malipo kwa watu wenye uhitaji nchini. Waziri Ndumbaro alitoa msaada wa kisheria kwa wafungwa 15 na mahabusu wawili katika gereza hilo, huku akisisitiza umuhimu wa haki kwa wale waliodhulumiwa au kufungwa kwa makosa ya kusingiziwa.
Amesema kampeni hiyo imekwishafikia jumla ya mikoa 11, huku mpango ukiwa ni kuifikia mikoa yote nchini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025. Tayari huduma hizi zinatolewa katika mikoa ya Iringa, Mara, Songwe, na Morogoro, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki na msaada wa kisheria unaostahili.