Serikali kuchunguza shisha kuchanganywa na dawa za kulevya

0
31

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya amesema Serikali inafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama dawa za kulevya zinawekwa kwenye shisha katika baadhi ya kumbi za starehe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 25, 2023 jijini Dodoma katika maadhimisho ya wiki ya sheria, Kusaya amebainisha kuwa wanafanya uchunguzi huo ikiwa inatumika ndivyo sivyo katika baadhi ya maeneo nchini.

“Shisha sio madawa ya kulevya ila ikatokea mtu akaweka dawa za kulevya kwenye shisha hilo ni kosa. Sisi hizo taarifa tunazo tunaendelea kuzifanyia kazi kwa kutumia mamlaka husika,” amesema Kusaya.

Aidha, amesema bado kuna changamoto ya matumizi ya dawa za binadamu zenye asili ya kulevya kutumika kama mbadala wa dawa za kulevya akitolea mfano wa dawa ya Ephedrine inayotumika kutibu kifua, Ketamine inayotumika kuondoa maumivu kwenye operesheni na ipo ya aina mbili ya vidonge na maji, Tramadol inayotumika kuondoa maumivu na valium kutibu mafua na kupata usingizi.

“Wanatumia kwa sababu wanakosa kile anachokihitaji, hizi dawa zikitokea bahati mbaya matumizi yakawa makubwa mtu anaweza kupoteza maisha,” amesema Kusaya.

Send this to a friend