Serikali kuendeleza mabonde ili kukabiliana na mafuriko nchini

0
16

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea na mpango wa kuyaendeleza mabonde nchini kwa kuyatumia kutoa huduma za kijamii ikiwemo upatikanaji wa maji na nishati ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na mafuriko.

Amesema moja ya mkakati uliochukuliwa na Serikali ni kuunda mamlaka za mabonde zenye wajibu wa kufanya ufuatiliaji wa mwenendo upitishaji maji na kuratibu namna nzuri ya utumiaji wa mabonde hayo.

Amesema hayo leo Aprili 24, 2025 wakati akijibu swali la mbunge wa Kyela, Ally Jumbe aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kukabiliana na mafuriko nchini, wakati wa kipindi cha maswali ya wabunge kwa Waziri Mkuu.

“Kama ambavyo tumeona kwenye bonde la mto Rufiji, tumeamua kuanzisha mradi mkubwa sana wa kuzalisha umeme. Nilifanya ziara mkoani Morogoro ambapo tunachimba bwawa kubwa ambalo linategemea maji ya mto Ruvu; ujenzi wa mabwawa haya yataleta maslahi kwa Watanzania ikiwemo kwenye sekta za kilimo, nishati, maji na mifugo.”

Ameongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha inaongeza bajeti kwenye Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). “Tunataka kuhakikisha maji yanayosababishwa na mvua hayapotei bure bali tunayatumia kwa faida ya Watanzania.”

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kusimamia maslahi ya watumishi, mishahara na madai mbalimbali ili kuhakikisha yanalipwa kwa wakati na waweze kuendesha maisha yao.

Send this to a friend