Serikali kufanya mabadiliko ya Sheria ya Vyombo vya Habari

0
62

Serikali ya Tanzania inakusudia kufanya mabadiliko ya baadhi ya vifungu vya sheria zinazosimamia vyombo vya habari ili kuvifungulia vyombo vyote vilivyofungiwa kwa nyakati tofauti kutokana na makosa mbalimbali.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju amesema kuwa serikali imeendelea kufanya mazungumzo na wamiliki wa vyombo vya habari na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania (THRDC) kuhusu suala hilo.

Ameongeza kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameielekeza wizara huyo kutatua changamoto ya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Wakati wa maadhimisho Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mei 3 mwaka huu, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kilikosoa Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Habari 2016 na kanuni ya maudhui ya kimtandao, kuwa zina vifungu amabvyo havijakidhi viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza.

TAMWA imesema Uhuru wa Vyombo vya Habari na wanahabari ni moja ya haki ya msingi ya kiraia ambayo huwapa jamii haki yao ya kupata habari na kusambaza taarifa, haki ya uhuru wa kujieleza pamoja na haki ya uhuru wa maoni ambazo ni haki za msingi katika mataifa yanayojiendesha kwa misingi ya demokrasia.