Serikali kufanya uhakiki wa raia wa kigeni walioajiriwa shule binafsi

0
39

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amezitaka shule binafsi kuacha tabia ya kuajiri walimu na wafanyakazi wa kigeni katika shule zao bila kufuata utaratibu za kupata vibali.

Prof. Ndalichako amesema kuwa watakwenda kufanya uhakiki katika shule hizo na watakao wabaini watachukuliwa hatua za kisheria.

Prof. Ndalichako ametoa onyo hilo jijini Dodoma wakati akifunga mkutano wa 15 wa wakuu wa shule za Sekondari uliofanyika jijini hapo kwa siku tatu kwa lengo la kutathmimni changamoto na mafanikio waliyoyapata kwa mwaka mzima katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, amewataka wakuu hao wa Shule kwenda kusimamia ulinzi na usalama wa maeneo ya shule ikiwamo kudhibiti majanga ya moto ambayo yameibuka kwa wingi katika siku za hivi karibuni kwa mabweni ya wanafunzi kuungua.

“Wakuu wa shule ndio wasimamizi wa kila kitu katika maeneo ya shule siku za hivi karibuni yameibuka maswala ya moto katika mabweni ya wanafunzi kuungua mkasimamie hayo kwa ukaribu sana majanga kama hayo yasijirudie tena,” amesema.

Ndalichako ametumia jukwaa hilo kuwaonya baadhi ya maafisa elimu wasio waminifu ambao amesema hushiriki vitendo vya wizi wa mitihani ili kuonekana katika maeneo yao ufaulu upo juu na pindi inapogundulika kuwasingizia wakuu wa shule.

Awali, Rais wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Mwalimu Frank Mahenge amesema katika mkutano huo wametumia kutathmini utendaji wao wa kazi kwa mwaka unaoisha na wameshirikisha changamoto wanazokutana nazo katika maeneo yao ya kazi sambamba na kuweka mikakati mipya ya kwenda kutekeleza kwa mwaka ujao.

Send this to a friend