Serikali kuhamisha shughuli zote za mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa TTCL
Serikali imesema ipo katika mchakato wa kuhamishia shughuli zote za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye katika kikao kazi na wakandarasi wajenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano jijini Dodoma.
“Kama nilivyozungumza Bungeni wakati wa wasilisho la hotuba ya Bajeti ya Wizara hii Mei 20, 2022 kuwa tupo katika mchakato wa kuhamishia shughuli zote za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Shirika letu la TTCL. Wizara imeulea mpaka umekuwa na sasa upo tayari kukabidhiwa kwa Shirika hilo,” amezungumza Waziri Nape.
Ameongeza kuwa, hana mashaka na uwezo wa Mkurugenzi wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga katika kusimamia shughuli zote za mkongo, pia ana matumaini makubwa kuwa ataweza kubeba jukumu hilo pindi mchakato huo utakapokamilika.
Hata hivyo, TTCL imekabidhiwa nyaraka zenye michoro ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliokamilika ambazo ni kilomita 72 kutoka Mangaka-Mtambaswala, na kilomita 105 za Arusha-Namanga, kwa ajili ya kuliwezesha shirika kusimamia na kuendesha mkongo huo.