
Serikali imedhamiria kuboresha Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuijenga upya ili kuwezesha huduma zote kutolewa ndani ya jengo moja litakalokuwa na vitanda 1,757 kutoka 1,435 vya sasa ambapo mradi huo utagharimu Dola za Marekani milioni 468 [takriban TZS trilioni 1.2] ambapo kati ya fedha hizo USD milioni 364 zitatoka Korea Kusini na Serikali ya Tanzania itachangia USD milioni 104.
Akizungumza Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Rachel Mhaville kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya mafanikio ya kipindi cha miaka minne chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu, amesema kwa sasa upembuzi yakinifu wa mradi huo umekamilika hivyo hatua mbalimbali za kusaini mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Korea zinaendelea vizuri.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni wa awamu moja ambao utachukua miaka mitano kukamilika baada ya kusaini mkataba, akieleza kuwa hatua hiyo haitaathiri utoaji wa huduma hospitalini hapo, hivyo huduma zitaendelea kutolewa kama kawaida.
“Utekelezaji wa mradi huu wa kihistoria katika sekta ya afya nchini na Ukanda wa Afrika, utakua na faida lukuki ikiwemo kuboreshwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kupitia vifaa tiba vya kisasa na kwamba Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, kuwezesha wagonjwa kupata huduma zote katika eneo moja, kupunguza mizunguko na usumbufu pamoja na kuwa na mpangilio mpya wa hospitali huku eneo kubwa likibaki wazi kwa matumizi ya maendeleo mengine miaka 50 ijayo,” amesema Dkt. Mhaville.
Hospitali ya Taifa Muhimbili yenye kampasi mbili ni Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini ina vitanda 2,043 ambapo Upanga kuna vitanda 1,435 na Mloganzila vipo 608.Katika kampasi zote mbili wagonjwa 4,000 wanaonwa kwa siku.