Serikali kuimarisha ushirikiano kati ya wawekezaji na wananchi

0
9

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof.Kitila Mkumbo, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na wawekezaji pamoja na wananchi ili kuimarisha na kukuza uchumi wa Taifa, sambamba na kuinua kipato na ustawi wa mwananchi mmoja mmoja.

Prof. Mkumbo ametoa kauli hiyo leo, Februari 23.2026, wakati wa ziara yake mkoani Morogoro, katika Kata ya Matuli, ambako ametembelea kiwanda cha uwekezaji cha EAGLE AGROTECH pamoja na shamba la mazao ya nafaka la SANTAGRO LIMITED.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkumbo amepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazoendelea, ikiwemo uzalishaji wa mazao ya kilimo ya nafaka kama alizeti Mtama,Mahindi pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuongeza thamani ya mazao. ameeleza kuridhishwa na kasi ya uwekezaji unaoendelea katika sekta ya kilimo na viwanda, akibainisha kuwa sekta hizo ni nguzo muhimu katika safari ya mageuzi ya kiuchumi ya Taifa.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kuboresha miundombinu, kurahisisha taratibu za uwekezaji, na kuhakikisha sera na mipango ya maendeleo inalenga kuongeza tija, ajira na mapato ya ndani. Aidha, amewahimiza wawekezaji kuzingatia sheria, kulinda maslahi ya wafanyakazi pamoja na kushirikiana na jamii zinazowazunguka ili kuhakikisha maendeleo yanakuwa jumuishi na endelevu.

Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, Tanzania itaweza kuongeza uzalishaji wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, na kuongeza mauzo ya mazao na bidhaa katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kufuatilia na kuhimiza uwekezaji wenye tija katika sekta za kimkakati, hususan kilimo na viwanda, ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.

Send this to a friend