Serikali kuja na mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto

0
48

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kufikia mwaka 2025 Serikali inakusudia kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kujenga majengo ya mama na mtoto kwenye hospitali za rufaa kadhaa ndani ya Tanzania ikiwemo Mbeya, Njombe, Simiyu, Geita, Songwe, Katavi, Kilimanjaro, Mwanza, Morogoro, Tabora na Dar es Salaam.

Amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa jengo la afya ya mama na mtoto, CCBRT jijini Dar es salaam.

“Tunataka tuendelee kupunguza zaidi vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua. Kwa hiyo mbali na juhudi za sekta binafsi, taasisi au mashirika, Serikali nayo inafanya jitihada kubwa,” amesema.

Aidha, amesema katika mikakati ya kuboresha huduma kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga, Wizara kwa kushirikiana na vyama vya kitaalamu vya madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na uzazi, wameanzisha mfumo wa kupitia takwimu za vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua na kubaini kuwa asilimia kubwa ya wanaofariki ni kutokana na mapungufu ya watoa huduma.

Amemuagiza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu pamoja na sekretarieti yake kusimamia uzembe, dharau na na uangalizi hafifu wa watoa huduma pindi wanawake wapojifungua hospitalini ili kuzuia maafa makubwa.

Mbali na hayo Rais Samia ameipongeza taasisi ya CCBRT kwa utaratibu waliouanzisha kwa mama mjamzito kuingia katika chumba cha kujifungua akiambatana na mwafamilia, na kusema itasaidia akina baba kujua hali wanazopitia wake zao pamoja na kuunga mkono uzazi wa mpango.

“Hakuna wakati wa faraja kama wakati wa kujifungua ukiwa na mtu wako pembeni ambaye anasaidia kukupoza. Lakini hii [kuingia leba na mwanafamilia] itasaidia wanaume zetu kuona kishindo tunachopambana nacho kule ndani, na kwa maana hiyo watatusaidia kwenda kwenye uzazi wa mpango,” ameeleza.

Send this to a friend