Serikali kuja na mpango wa kuirejesha Tanzanite Tanzania

0
71

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameeleza kutoridhika na usimamizi wa uchimbaji na uuzaji wa madini ya Tanzanite unavyofanyika, hivyo ameaigiza Wizara ya Madini kuja na mpango ambao utaifanya dunia kutambua kuwa madini hayo ya kipekee yanapatikana Tanzania tu.

Rais Samia ametoa agizo hilo wakati akizungumza mara baada ya kuzindua kiwanda cha kusafisha dhahabu mkoani Mwanza, ambapo ameeleza kuwa bado Tanzanite haijawa yenye manufaa sana kwa nchi, na hiyo inatokana na kuwa inapatikana sehemu mbalimbali dunia, utadhani na wao huo wanaichimba.

“Tanzanite Mungu aliipendelea Tanzania pekee yake dunia nzima. Lakini tunavyokwenda sasa Tanzanite ni kama madini yanayochimbwa dunia nzima. Ukienda kwa majirani zetu kuna Tanzanite, nyingi tu, ukienda bara la Asia kuna Tanzanite nyingi tu, kotekote imesambaa dunia,” amesema Rais Samia akieleza masikitoko yake.

Kutokana na changamoto hiyo, Rais amesema kuna haja ya kukaa na kui-rebrand (kuitangaza upya) Tanzanite, ili kuipa upekee utakaoitambulisha kuwa inapatikana Tanzania tu.

Rais amependekeza kuwa kuwepo na mwamvuli mmoja ambao ndio utahusika kununua Tanzanite yote inayochimbwa, na utasimamia uuzaji wa madini hayo kimkakati, ili wananchi na Taifa wanufaike, kwani baada ya muda rasilimali hizo zitakwisha.

Mbali ja kuzindua kiwanda hicho ambacho kitatoa ajira, kukuza mapato ya serikali, kuongeza uchimbaji madini na kutoa fursa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kununua dhahabu , Rais ambaye yuko mkoani Mwanza kwa ziara ya siku tatu, leo katika siku yake ya kwanza anafungua pia jengo la BOT, Tawi la Mwanza.

Send this to a friend