Serikali kuja na mpango wa kupunguza gharama za bando
Serikali imesema inakuja na mpango wa kufanya uwekezaji mkubwa kwenye TEHAMA ili kupunguza gharama za uzalishaji utakaosaidia kushuka kwa bei za ‘Bando’ hapa nchini.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam , Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kwa Tanzania bado gharama za kuzalisha bando ni kubwa ukilinganisha na gharama ya bando inayouzwa.
Waziri amebainisha kwamba, kwakuwa Watanzania wengi hawana uwezo wa kumudu gharama hizo, Serikali inaongeza uwekezaji zaidi kwenye miundombinu ya kisasa ili kupunguza zaidi gharama za uzalishaji na kuwawezesha Watanzania kumudu.
Amefafanua kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa mkongo wa taifa ambao utapunguza gharama za bando mara utakapofika kwenye makazi ya watu.
“Mwaka huu fedha imetengwa kwa ajili ya hiyo, na tunaliwezesha Shirika letu la TTCL ikiwezekana waondoke kwenye shughuli za kawaida za mobile, waende kwenye kuwekeza kwenye miundombinu ya mawasiliano ili tupunguze gharama za uzalishaji wa data,” amesema Waziri Nape.