
Serikali imewezesha ujenzi wa shule mpya 103 za sekondari za amali ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kati ya shule hizo, shule 29 ni za amali za kihandisi na shule 74 ni za amali zisizo za kihandisi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo na kusisitiza kuwa kukamilika kwa shule hizo kutawezesha kuongezeka kwa idadi ya shule za amali za sekondari kutoka shule tisa hadi shule 112 za sekondari za amali.
Waziri Mkenda amesema sambamba na jitihada za kuongeza shule za sekondari za amali nchini, pia Serikali imeendelea kuongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya ufundi hadi kufikia wanafunzi 199,118 kwa mwaka 2024/25 ikilinganishwa na wanafunzi 161,750 waliodahiliwa kwa mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 37,368 sawa na asilimia 23.
Amesema ongezeko la udahili wa wanafunzi linatokana na kuongezeka kwa vyuo vya elimu ya ufundi hadi kufikia vyuo 512 kwa mwaka 2024/25 kutoka vyuo ufundi 441 mwaka 2021/22.
Waziri Mkenda amesema Serikali imedahili wanafunzi 11,232 kati ya 15,150 walioomba kujiunga na mafunzo ya Ufundi Stadi katika mwaka wa masomo 2025. Aidha, idadi ya wanafunzi katika vyuo vya mafunzo ya Ufundi Stadi – VETA imefikia wanafunzi 58,912 (wanawake 12,022 na wanaume 46,890) ambapo kati yao wanafunzi wa kozi za muda mrefu 24,670 (wanawake 8,450 na wanaume 16,220) na wa kozi za muda mfupi ni 34,242 (wanawake 3,572 na wanaume 30,670).
Amesisitiza kuwa ongezeko la wanafunzi linatokana na kuongezeka kwa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi (VET) kutoka 810 mwaka 2021/22 hadi kufikia Vyuo 905 mwaka 2024/25. Vilevile, imedahili wanafunzi 391 katika Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro – MVTTC ili kuongeza idadi ya walimu wa elimu ya ufundi.