Serikali kujenga vituo vya mafunzo kwa waraibu wa dawa za kulevya

0
39

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema  Serikali imejenga vituo maalum vya urekebu na ufundi stadi ili kuwasadia vijana  na wale wote wanaoathirika baada ya kutumia dawa za kulevya.

Ameyasema hayo leo bungeni  Dodoma  wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya dawa za kulevya ya mwaka 2022 ambapo amesema kwa mujibu wa utafiti unaonesha  uwepo wa kiwango kikubwa cha uzalishwaji na utumiaji wa bangi.

Waziri Mhagama amesema, kwa mwaka ujao wa  fedha 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya TZS Bilioni 8.7  zitakazotumika kujenga vituo vya urekebu na ufundi stadi, vitakavyosaidia kubadilisha tabia za vijana wanaotumia dawa  za kulevya.

“Vituo hivyo vitakuwa na kazi kubwa ya kuwaondoa kwenye matumizi ya dawa na kuwapa shunguli nyingine watakazotakiwa kuzifanya zitakazotokana na shughuli za ujuzi, ambazo watafundishwa kwenye vitu hivyo,” amefafanua.

Ameongeza kuwa kupitia Wizara ya Kilimo Serikali itafanya utafiti ili maeneo yanayolima bangi kibiashara kama vile Kisimiri Juu mkoani Arusha, kusaidiwa kulima mazao mbadala badala ya zao hilo haramu.

Aidha, Waziri Mhagama ametaja baadhi ya  mikoa inayoongoza kwa kulima bangi nchini kuwa ni pamoja na Arusha, Manyara, Mara na Njombe, na kuitaja baadhi ya mikoa itakayojengwa vituo hivyo kuwa ni pamoja na Shinyanga, Kilimanjaro, Mwanza  na Arusha.

Send this to a friend